Siri ya Utajiri ni ubahili,hii ni kauli ambayo wengi wamekuwa wakiitumia, na hufanya zoezi la kutengeneza utajiri kupewa taswira hasi.
Kwa sababu ubahili ni kubana sana fedha na kujinyima, basi wengi huona hayo siyo maisha ya kuishi. Kwa nini ujitese kutengeneza utajiri wa baadaye badala ya kutumia fedha hiyo sasa na ukawa na maisha bora?
Hili ni swali ambalo wengi hujiuliza na lina mantiki kubwa. Kujitesa leo ili kuwa na maisha mazuri kesho siyo mpango mzuri. Lakini msingi wetu wa utajiri bado ni ule ule, matumizi yawe madogo kuliko mapato. Sasa unafikiaje hili huku ukiwa na maisha bora kabisa kwako, yasiyo ya kujitesa?
Hapa ndipo tunapaswa kujifunza kitu muhimu sana kuhusu fedha na matumizi, kipi unachojali wewe, kipi kinachokupa wewe furaha. Kwa kujua hayo, utaweza kudhibiti matumizi yako vizuri, huku ukiwa na maisha bora zaidi kwako.
Nadhani kila mtu amewahi kusikia kauli kwamba fedha haiwezi kununua furaha. Kauli hiyo huwa inatokana na tabia ya watu kuahirisha maisha, wakiamini wakishakuwa na fedha basi watakuwa na furaha, kitu ambacho huwa hakitokei.
Fedha na furaha ni maeneo mawili tofauti kwenye maisha, ambayo yanaweza yasiwe na uhusiano wa utegemezi. Unapaswa kuwa na furaha kabla hata hujawa na fedha.
Katika kujenga maisha bora na yenye furaha, angalia wewe unajali nini. Ni kitu gani ambacho unapenda sana kwenye maisha yako. Na hicho ndicho unachopaswa kutumia kipato chako kuhakikisha unakipata.
Hapo unaweza kufanya matumizi utakavyo, na kuweka juhudi kuhakikisha unapata kipato cha kukuwezesha kupata kile unachotaka. Vitu vingine vyote ambavyo havina maana kwako, unaachana navyo kabisa. Vitu ambavyo huvijali , usiruhusu kabisa vichukue sehemu ya kipato chako.
Kwa njia hii utapata kile ambacho unakifurahia, na kuachana na matumizi ambayo yanakuwa mzigo kwako, wakati hayana maana kwako. Ili kufanya zoezi hili lazima kwanza ujitambue wewe binafsi. Uaache kufanya maamuzi kwa kufuata kundi kubwa la watu wanafanya nini. Badala yake uwe unafanya kile ambacho unakijali wewe, kile ambacho ni muhimu kwako na kina maana kwako.
Kwa kufanya hivi, kwa nje bado watu wataona wewe ni bahili, kwa sababu watu wana maana zao wenyewe za namna gani kila mtu anapaswa atumie fedha zake. Bado watu watasema una maisha ya ajabu kwa sababu huishi kama wanavyotaka wao, lakini hilo halitakuwa na shida kwako kwa sababu unafanya kile unachojali, na siyo kuwaridhisha watu. Kwako wewe hautakuwa ubahili bali maisha ambayo yana maana kwako, na hii ndiyo itakayokutofautisha wewe na wengine kifedha.
Changamoto kubwa kwa watu wanaopata fedha ni kuwa watumwa wa watu wengine. Kutaka kuishi kama vile ambavyo watu wengine wenye fedha kamazao wanavyoishi. Na hili ni moja ya vikwazo kwa nini wasomi wengi huwa hawafikii uhuru wa kifedha.
Kwa sababu wengi hufanya mambo ambayo yapo nje ya uwezo wao, kwa sababu ya msukumo ya wale wanaowazunguka. Inahitaji nidhamu ya hali ya juu na kujitoa kweli kama unataka kuishi maisha ambayo yana maana kwako na siyo mzigo kwako.
Moja ya watu matajiri sana ambao wanasemekana ni mabahili ni Bilionea Warren Buffet, ambaye ni tajiri mkubwa wa kipindi kirefu. Mwaka 2017 utajiri wake ulikuwa unakadiriwa kuwa dola bilioni 77. Ukiipeleka hiyo mwaka huo kwenye fedha za kitanzania ni trilioni zaidi ya 150, bajeti ya nchi kwa miaka karibu hata kumi kipindi hicho.
Pamoja na utajiri huo mkubwa, Buffet bado alikuwa anaishi kwenye nyumba yake aliyonunua mwaka 1958 huko OMAHA, Nebraska nchini marekani. Alikaa kwenye nyumba moja kwa miaka 61, na alipoulizwa kwa nini pamoja na utajiri mkubwa bado maisha yake ni ya kawaida , jibu lake lilikuwa ni kwamba mafanikio kwake ni kufanya kile kitu anachopenda , nay eye anapenda kuwekeza. Hivyo anafanya kile anachopenda, na vingine anaachana navyo.
Siyo lazima maisha yako yawe kama Warren Buffet, lakini najua umepata ninachotaka kukuonesha hapa, kwamba ishi maisha kwa kujali vile ambavyo vina maana kwako, vile ambavyo unapenda, siyo kujibebesha mizigo kwa kufanya mambo ili kuwaridhisha watu wengine. Kwa sababu fedha unayotumia kununua vitu usivyojali, ukiiwekeza miaka 20 ijayo itakuwa imeongezeka thamani sana.
Sasa inashangaza unaposoma makala au kitabu kimoja, unapata hamasa na kuona umeshamaliza kila kitu.
Hapo unajidanganya na kujiweka kwenye hatari ya kuishia njiani.
Unapaswa kuendelea kuchochea hamasa yako kila siku kwa kuendelea kujifunza bila kuchoka au kuona umeshajua kila kitu.
Kila siku jifunze vitu vipya na vinavyokusukuma kupiga hatua zaidi.
Kuendelea kuchochea hamasa yako ya kufanikiwa, kila siku tembelea www.amkamtanzania.com
Au fungua www.somavitabu.co.tz.
Baada ya kujua jinsi ya kudhibiti matumizi yako na bado ukawa na maisha bora, kuna rasilimali muhimu unapaswa kuwa nazo ili kufanikiwa.
- Kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, ambacho kitakusaidia kujitambua.
- Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, kitakusaidia kuweka akiba na kuwekeza.
- Kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI, kitakachobadili mtazamo wako kwa ujumla.
- Kitabu cha MIMI NI MSHINDI, kitakachokufundisha kuishi kwa ushindi kila siku.
- Jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, itakayokusukuma kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kupata rasilimali hizi wasiliana na 0752977170.
Nikutakie kila la kheri kwenye safari hii ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.