Katika vipindi vyote ambavyo binadamu wameishi hapa duniani, miaka mingi sana mpaka kufikia sasa, hakuna kipindi kizuri kuingia au kuwa kwenye biashara kama kipindi tunachoishi sasa.
Ni upendeleo wa kipekee kwetu sisi kuwa hai kipindi hiki na kama tutashindwa kukitumia vizuri basi tutakuwa tumejiungusha sisi wenyewe.
Hebu fikiria kipindi cha zamani ambapo watu walikuwa ni wakulima au wafugaji tu. Kipindi ambacho watu walihitaji kulima shambani kwa jembe la mkono siku nzima huku jua likiwawakia.
Wakitumia mbegu ambazo sio bora sana na hivyo kupata mavuno kiduchu. Na hata baada ya kupata mavuno hayo, alipotaka kupata mboga ya tofauti ilimbidi kutoa sehemu ya mazao yake ndio apate mboga.
Kwa mfano kama alitaka kula mbuzi, basi ilimbidi kutoa gunia la mahindi (kama yeye ni mkulima wa mahindi) ndio aweze kupata huyo mbuzi.
Fikiria kipindi ambacho hakukuwa na simu, hakukuwa na umeme, hakukuwa na kompyuta wala hakukuwa na mtandao wa intaneti.
Mawasiliano yalikuwa kupitia barua ambayo kuituma mpaka upokee majibu ilikuwa inachukua miezi. Lakini njoo kwenye ulimwengu tulionao sasa. Ukuaji wa teknolojia umerahisisha sana mawasiliano na muingiliano wa binadamu.
Leo hii unaweza kufanya mambo mengi ambayo usingeweza kuyafanya kabisa miaka 10 tu iliyopita. Leo hii unaweza kufanya biashara ya kitaifa na hata ya kimataifa kwa kuanza na mtaji kidogo kabisa. Leo hii unaweza kuwasiliana na mtu aliyepo popote duniani ndani ya sekunde chache tu.
Zamani kidogo ulihitaji mtaji mkubwa sana ili uweze kuingia kwenye biashara. Kwanza biashara zilikuwa ni chache na hivyo watu wachache waliweza kuzihodhi. Kama hukuweza kujenga kiwanda, au kuwa msambazaji mkubwa wa bidhaa au kuwa muuzaji unayejulikana sana, hukuwa na nafasi ya kuweza kufanikiwa kwenye biashara.
Fursa zilikuwa chache na ushindani ulikuwa mkali. Na hata ungeonesha utofauti wako, watu wangekuwa tayari kufanya chochote kuhakikisha wanakuondoa kabisa sokoni. Sasa hivi mambo yamebadilika,unaweza kuanza biashara bila hata ya kuwa na mtaji kabisa.
Kwa kutumia mazingira uliyonayo, vipaji vyako na elimu au uzoefu ulionao unaweza kupata mambo mengi sana ya kufanya. Mtandao wa intaneti umerahisisha shughuli zote za kibiashara. Mtu anaweza kufungua duka lake kwenye intaneti na akauza bidhaa au huduma zake. Mtu anaweza kutumia intaneti kutangaza bidhaa au huduma zake na akatengeneza soko la kutosha.
Tunaishi kwenye wakati ambao hakuna tena bidhaa moja ambayo inatawala soko. Pia hakuna tena soko moja ambalo kila mtu analitupia jicho. Tuna bidhaa nyingi ambazo zipo sokoni na tuna masoko mengi pia. Kila mfanyabiashara makini anaweza kutengeneza soko lake ambalo hawezi kubughudhiwa na mtu mwingine yeyote.
Kipindi tunachoishi ni kipindi ambacho biashara zinafanyika kwa kujenga ushirikiano na ushirikiano huu ndio unazaa masoko madogo madogo ambapo hata wewe unaweza kuingia hapo na kutengeneza soko lako kulingana na bidhaa au huduma unayotoa.
Wakati huu pia vyanzo vya fedha zakuanzisha na kukuza biashara vimekuwa vingi na rahisi kupatikana. Tofauti na zamani ambapo taasisi za kifedha zilikuwa chache na zilikuwa zinahudumia watu wenye biashara kubwa tu, sasa hivi kuna taasisi za kifedha nyingi na hivyo kila ambaye anahitaji huduma za kifedha anaweza kuzipata.
Elimu pia inapatikana kwa urahisi kipindi hiki. Zamani ingekuhitaji ukasome chuo ndio uweze kupata elimu ya biashara na ambayo isingekuwezesha kupambana na changamoto halisi za kibiashara. Ila sasa hivi unaweza kupata elimu kiurahisi zaidi na inayoendana na uhalisia wa biashara unayofanya au unayotaka kufanya. Elimu kama hii unayoipata hapa ingekuwa vigumu sana wewe kuipata miaka 20 iliyopita.
Huu pia ni wakati ambao Ajira zimekuwa tabu sana kupatikana. Watu wengi wamesoma ila nafasi za ajira ni chache. Uhaba huu wa nafasi za Ajira unawafanya waajiri wawe na nguvu zaidi na hivyo wafanyakazi kukosa nguvu ya kutetea maslahi yao. Hivyo kama umesoma na Ajira hakuna unafanya nini? Biashara. Kama umeajiriwa na kipato chako hakikutoshi, mwajiri wako hana dalili zozote za kukuongezea kipato, unafanya nini? Biashara.
Tuna kila sababu ya kutumia wakati huu vizuri, kutumia fursa zote zilizopo mbele yetu kuweza kuanzisha, kukuza na kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara.
Wewe unaweza kufanikiwa sana kupitia biashara unayofanya au unayotaka kufanya, pata maarifa sahihi na weka juhudi kubwa. Hakuna wa kukuzuia bali wewe mwenyewe.
Karibu upate vitabu mbalimbali kwa kufungua www.amkamtanzania.com/vitabu na www.t.me/somavitabutanzania.