Wewe siyo wa kwanza kupitia magumu unayopitia haupo mwenyewe, amka endelea na mapambano.
Ilikuwa ni majira ya saa nane mchana ,Msichana akiwa anamwendesha baba yake ambaye aliketi siti ya nyuma.
Baada ya maili chache mbele Kimbunga kikatokea..
Msichana akamuuliza baba yake, tunapaswa kufanya nini baba?
Baba akamjibu, ENDELEA KUENDESHA..
Mita chache mbele aliona magari mengine yakipaki pembeni kupisha kimbunga..
Msichana akapatwa na wasiwasi akamuuliza baba yake, Tunapaswa na sisi kupaki pembeni ?
Baba akamjibu, Hapana ..ENDELEA KUENDESHA..
Kuona hivyo akaanza kuendesha gari pole na kumwambia baba yake , Baba.. Nafikiri ninapaswa kupaki sasa hivi kwa sababu sioni mbele vizuri vumbi limetanda kwenye kioo.
Msichana aliendelea kumwambia baba yake, kimbunga kipo mbele yetu na ni hatari na kila mtu anapaki gari pembeni.
Baba yake akamwambia, ENDELEA KUENDESHA..
Wakati akiendelea kuendesha gari, Kimbunga kilikuwa kimetanda wingu zima.
Ikawa ni ngumu mno kwa msichana kuona vizuri mbele.
Alihisi kama anapaswa kupaki gari pembeni kwa usalama zaidi, baba aliendelea kumsisitizia ENDELEA KUENDESHA..
Aliendelea kuendesha licha ya kuwa na wasi wasi.
Ghafla alianza kuona vizuri kuliko mwanzo.
Baada ya maili chache kimbunga kiliisha.
Baba akamwambia, Mwanae .. sasa hivi unaweza kupaki pembeni na kutoka nje..
Msichana akajibu, Lakini kwa sasa hivi hakuna kimbunga.
Baba akatabasamu na kumwambia mwanae, Unapotoka nje , unaweza kuwaona waliokata tamaa na wale wanaoendelea kupambana na kimbunga.
Kamwe usikate tamaa songa mbele na kwa sababu hujakata tamaa kimbunga sasa hivi kimeisha.
Tunajifunza Unapopitia magumu kwenye maisha yako ujue umekaribia kufanikiwa usiishie njiani piga moyo konde songa mbele, hofu ni adui mkubwa wa mafanikio.
Kipindi kigumu hata watu imara huwa wanakata tamaa kama utaweza kuishinda hofu na kusonga mbele bila kukata tamaa utaweza kuvuka vikwazo na magumu yote unayopitia.
Rafiki yangu,
Leo napenda kusema na wale wanaopitia magumu kwenye maisha yao.
Wale ambao wanafikia hatua ya kujiuliza kama kweli wanajua wanachotaka na maisha yao.
Wale ambao mbele wanaona giza, wasijue kama wataweza kuvuka giza hilo na kubaki salama.
Hawa ndiyo watu ninaowataka hapa, na kama wewe siyo mmoja wao ila unapenda kuendelea kusoma soma, lakini mwishoni fikiria watu unaowajua wanaopitia magumu kisha watumie ujumbe huu muhimu sana kwao, ambao unaweza kuyabadili maisha yao kwa kiasi kikubwa sana.
Kwa kuanza, nikukumbushe hili muhimu rafiki yangu;
Siku utakayotangaza au kujiambia kwamba unataka kuwa na mafanikio kwenye maisha yako, unataka kufanya makubwa na kupiga hatua, itakuwa ndiyo siku umetangaza vita na dunia nzima.
Utakuwa umetangaza vita kubwa sana , ambayo kwa upande wako unakuwa mwenyewe, lakini upande wa pili kuna dunia nzima, kuanzia asili yenyewe, wale wanaokuzunguka na hata dunia nzima.
Unapochagua kufanikiwa, unakuwa umetangaza vita na wewe mwenyewe, umetangaza vita na ndugu, jamaa na marafiki, umetangaa vita na tv, redio, magazeti, facebook, instagram na kila aina ya chombo cha habari na mitandao ya kijamii.
Sasa vita hii haitakuwa rahisi, kwa sababu unaopambana nao, wana ,mbinu nyingi za kukurudisha nyuma.
Kama ni ndugu wa karibu na hata wazazi watakuambia usijiumize, endelea na maisha yako ya kawaida na usikazane na makubwa. Kwa upande wa marafiki na jamaa watakuambia usikazane sana, ili usiwaache wao. Dunia itakuonesha kila aina ya hatari iliyopo mbele yako kwa kile unachojaribu, halafu vyombo vya habari na mitandao ya kijamii itakuwa inafanya kila hila ya kupumbaza akili zako, ili usiweke muda wa kutosha kwenye kile unachofanya.
Rafiki, unaona sasa jinsi vita hii ilivyo ngumu?
Sasa ugumu bado hatujaufikia, ugumu halisi unakuja hapa; UTASHINDWA, UTAANGUKA.
Na hapo ndipo dunia itakucheka zaidi, ndipo watakuambia si tulisema, tulikuambia huwezi, tulijua utashindwa. Utakuwa na mashahidi wengi watakaotoa kila aina ya ushahidi dhidi yako, wakionesha jinsi ambavyo huwezi na utashindwa.
Huu ndiyo wakati ambao unahitaji kuwa imara sana, unahitaji kuwa na kitu kikubwa kinachokufanya uendelee na mipango yako, licha ya kupitia wakati mgumu.
Ninachotaka kukuambia leo rafiki yangu ni hiki, kila mtu unayemwona amepiga hatua na kufanikiwa, jua alipitia wakati mgumu. Jua alikutana na changamoto kubwa ambazo ziliwakatisha tamaa wengine lakini yeye aliendelea kuweka juhudi.
Rafiki, changamoto unazokutana nazo ni faida kwako, kwa sababu changamoto hizi zinawazuia wale ambao hawajajitoa kweli kufanikiwa, hivyo unabaki na uwanja mpana wa kuweza kufanikiwa kama utaweza kuvuka magumu unayokutana nayo.
Rafiki, pale unapojiona kwamba umefika ukingoni, pale unapoona hakuna tena namna ya kuendelea, hapo ndipo unapaswa kuendelea zaidi.
Pale unapoona umefika ukingoni, jiambie unahitaji kuweka juhudi kidogo zaidi ya wengine.
Angalia kwenye mashindano ya riadha, tofauti ya mshindi wa kwanza na wa pili huwa ni sekunde kadhaa tu, lakini zawadi zina u tofauti mkubwa.
Kwenye chochote unachojaribu kufanya , utakutana na magumu, utakutana na changamoto kubwa, watu watakuwa tayari kukuambia huwezi na hutashindwa.
Usikubali kumsikiliza yeyote anayekukatisha tamaa, na usikubali ugumu wowote uwe kikwazo kwako kupata chochote unachotaka.
Ubishi, uvumilivu, ung’ang’anizi ni muhimu sana katika kufikia malengo makubwa uliyojiwekea. Na kila unaposhindwa shukuru, maana kwenye kila unachoshindwa kuna somo muhimu sana unalopaswa kujua ili kufanikiwa zaidi.
Nimalizie kwa kusisitiza hili rafiki, mambo hayatakuwa rahisi, na watu hawatakuachia kirahisi ufanye unachotaka kufanya. Unahitaji mtu mmoja tu wa kukuruhusu wewe ufanye unachotaka, na mtu huyo ni wewe mwenyewe. Maana ukishajiwekea wasiwasi wewe mwenyewe, kila utakapokutana na kushindwa utakimbilia kuacha na kukata tamaa. Lakini kama umejitoa, na hujui kuhusu kushindwa, dunia itakuacha upate unachotaka, na wale wanaokukatisha tamaa watakuwa mashabiki wako.
Endelea kupambana rafiki yangu, wakati mgumu haudumu, ni kipindi kifupi cha kujifunza na kuwa bora zaidi.
Kama unapitia magumu kwenye maisha yako unaweza kuibadili hali hiyo kwa kusoma vitabu mbalimbali hapa (www.amkamtanzania.com/vitabu na www.t.me/somavitabutanzania.) , ambavyo vitakupa maarifa sahihi yatakayokuvusha salama kwenye magumu unayopitia.
Anza na maarifa sahihi kisha chukua hatua.
Rafiki yako anayekupenda sana,
Sir Rama|Copywriter| |Sales Officer Of Soma Vitabu Tanzania|.
Tuendelee Kujifunza….